SEQUIP-AEP
UJUE MRADI WA KUIMARISHA UBORA WA ELIMU YA SEKONDARI
SECONDARY EDUCATION QUALITY IMPROVEMENT PROJECT (SEQUIP)
PROGRAMU YA ELIMU YA SEKONDARI KWA NJIA MBADALA
ALTERNATIVE EDUCATION PATHWAY (AEP)
1.0 UTANGULIZI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imeandaa mradi wa miaka mitano (5) (2020/2021-2025/2026) wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini unaofahamika kwa kifupi kama SEQUIP. Katika mradi huu TEWW imepewa jukumu la kuimarisha utolewaji wa Programu ya Elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala unaofahamika kama SEQUIP-AEP kwa wasichana waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali.
2.0 MALENGO YA MRADI WA “SEQUIP-AEP”
Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha ubora wa elimu ya Sekondari inayotolewa kwa njia mbadala.
2.1 Malengo mahsusi
Malengo mahsusi ya mradi huu ni pamoja na;
a) kuongeza ufikiwaji wa wasichana walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, hali duni ya maisha au kupata ujauzito ambapo mradi umelenga kuwafikia wasichana wapatao 12,000 nchini kote.
b) kuwapatia wasichana mazingira bora ya kujifunzia, na
c) kuboresha uhitimu bora wa elimu ya sekondari kwa walengwa.
3.0 Walengwa wa Mradi
Walengwa wa mradi huu ni wasichana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 20 waliokatisha masomo ya elimu ya programu ya elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali. Mradi huu unatoa fursa kwa mara nyingine kwa wasichana hao kuweza kuendelea tena na masomo yao ya elimu ya sekondari na hatimaye kufikia malengo yao waliyojiwekea.
4.0 Utaratibu wa Kujiunga na Programu
Mlengwa mwenye sifa anapaswa kujaza fomu ya maombi ya kujiunga na programu ya elimu ya sekondari kwa njia mbadala ambayo inapatikana katika ofisi za mikoa za TEWW zilizopo katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Aidha, fomu pia inapatikana katika tovuti ya TEWW ambayo ni www.iae.ac.tz. Mara baada ya kumaliza kujaza fomu hiyo inatakiwa kurejeshwa kwenye ofisi ya TEWW kwenye Mkoa uliopo. Aidha serikali itagharamia malipo ya ada kwa wanafunzi hao. Kwa mawasiliano zaidi unaweza kuwasiliana na Mratibu wa Mradi wa SEQUIP-AEP kupitia namba ya simu 0766968470.