Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, leo Machi 26, 2026 ameongoza uwasilishaji wa mada kuu (Keynote presentations) katika Kongamano la Kimataifa la Maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala, linalobeba kaulimbiu isemayo “Transforming Education for Sustainable Development.” Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu wa elimu, watunga sera na wadau kutoka ndani na nje ya nchi, ili kujadili mwelekeo wa elimu unaoendana na mahitaji ya sasa.
Katika kongamano hilo, mada muhimu zimewasilishwa zikijikita katika maeneo ya kimkakati ikiwemo elimu jumuishi na elimu kwa wote, matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) katika kujifunza na kufundisha, pamoja na maadili ya ualimu na taaluma (professionalism). Mada hizi zinaakisi mabadiliko yanayohitajika katika mfumo wa elimu ili kuendana na kasi ya teknolojia na kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
Kongamano hilo la siku tatu linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilifunguliwa rasmi Machi 25, 2026 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi. Dkt. Emmanuel Nchimbi, na linatarajiwa kuhitimishwa Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam. Kupitia jukwaa hilo, wadau mbalimbali wa elimu wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili kwa kina masuala yanayohusu maboresho ya sera na mitaala ya elimu, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa elimu nchini na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.