TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MKUU WA TEWW AFANYA ZIARA TANGA KUKAGUA UJENZI WA KARAKANA
MKUU WA TEWW AFANYA ZIARA TANGA KUKAGUA UJENZI WA KARAKANA
02nd Jun, 2025

MKUU WA TEWW AFANYA ZIARA TANGA KUKAGUA UJENZI WA KARAKANA

 

Na TEWW - Tanga

 

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga amefanya ziara ya kikazi Mei 27, 2025 mkoani Tanga kujionea maendeleo ya karakana nne (4) zinazojengwa mkoani humo.

 

Katika ziara hiyo Prof. Sanga alitembelea karakana ya mfano inayojengwa Jijini Tanga na karakana nyingine za kawaida zinazojengwa Shule ya Msingi Magila (Halmashauri ya Muheza); Shule ya Msingi Ndeme (Halmashauri ya Lushoto); na Shule ya Msingi Makasini (Halmashauri ya Kilindi).

 

Ujenzi wa karakana hizo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya mpango changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu (IPOSA) inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia shirika la KOICA.

 

Kwa mujibu wa Prof. Sanga ziara hiyo ililenga kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa karakana hizo ambazo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza elimu ya ujuzi kwa watu wazima na vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.

 

Katika ziara hiyo Prof. Sanga aliambatana na Dkt. Sempeo Siafu (Mratibu wa IPOSA TEWW) pamoja na wawakilishi kutoka taasisi kadhaa zinazotekeleza programu ya IPOSA. Miongoni mwa wawakilishi hao na taasisi zao katika mabano ni: Bi. Felister Mapunda (Mratibu wa IPOSA WyEST); Bw. Sedet Bulaya (Mratibu wa IPOSA OR-TAMISEMI); na Bi. Efratha Kristos (mwakilishi wa GDC iliyo chini ya KOICA).

 

Tanga ni miongoni mwa mikoa sita (6) nchini inayofaidika na programu ya IPOSA inayolenga kuboresha stadi za maisha na kuongeza fursa za ajira kwa vijana na watu wazima kupitia elimu kwa vitendo, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya mtu binafsi, jamii, na taifa kwa ujumla.