TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
02nd Mar, 2026

‎Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga leo Machi 2, 2026 amepokea ugeni wa Afisa Mwandamizi, Aminata Tamboura kutoka Makao Makuu ya DVV International nchini Ujerumani. Afisa huyo aliambatana na Frauke Heinze ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa Kanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika na kufanya nao mazungumzo ya kimkakati kuhusu kuimarisha utekelezaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini. 

‎Mazungumzo hayo yalilenga mipango ya pamoja na mwelekeo wa mageuzi ya sera na mahitaji halisi ya kijamii na kiuchumi, kwa kuzingatia mchango wa elimu katika kujenga ujuzi, ajira na ustahimilivu wa jamii.

‎Katika kikao hicho, pande zote zimekubaliana kushirikiana kufanya mapitio ya Mkakati wa Kisomo na Elimu kwa Umma (NALMERS) ili iendane na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mahitaji ya sasa. Aidha, wamekubaliana kuendeleza maboresho ya Mfumo wa Tuzo wa Taifa (Tanzania Qualifications Framework) kwenye sekta ndogo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, ambapo kwa awamu ya kwanza wataandaa miongozo ya utekelezaji wa utambuzi wa ujuzi na maarifa yanayopatikana nje ya mfumo rasmi (Recognition of Prior Learning – RPL).