TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
PROF. SANGA ASISITIZA VYUO VYA BIBLIA KUFANYA MAGEUZI YA KUJUMUISHA MAFUNZO YA AMALI
PROF. SANGA ASISITIZA VYUO VYA BIBLIA KUFANYA MAGEUZI YA KUJUMUISHA MAFUNZO YA AMALI
02nd Mar, 2026

‎Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

‎Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesisitiza umuhimu wa mageuzi ya kimkakati katika vyuo vya Biblia ili viweze kuchangia kikamilifu ujenzi wa jamii endelevu. Akizungumza Februari 28, 2026 wakati wa uzinduzi wa mtaala ulioboreshwa wa Chuo cha ABC Bible College & Training Center, Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Prof. Sanga alisema taasisi za kidini zinapaswa kupanua wigo wa mafunzo yao kwa kuunganisha theolojia na elimu ya ujuzi, ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwajengea wanajamii uwezo wa kujitegemea kiuchumi, kijamii na kimaadili.

‎Alieleza kuwa kupitia mafunzo yaliyoandaliwa kwa mtazamo mpana, jamii itajengewa uwezo wa kuchambua na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikumba kijamii ikiwemo umaskini, afya na ukosefu wa ajira kwa weledi na mbinu za kitaalamu. Alisisitiza kuwa kujifunza ni mchakato endelevu unaohitaji unyenyekevu, akibainisha kuwa sifa ya msingi ya kiongozi wa kiroho ni utayari wa kuendelea kujifunza na kubadilishana maarifa kwa manufaa ya wengine.

‎Prof. Sanga alifafanua kuwa jukumu la chuo si tu kufundisha nadharia, bali kuibua, kukuza na kusimamia vipawa na karama zilizopo ndani ya kila mnufaika.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Askofu Flaston Ndabila, alisema maboresho ya mtaala yamepanua wigo kutoka theolojia pekee na sasa yanajumuisha ujasiriamali, stadi za maisha, kompyuta, afya ya jamii na elimumsingi kwa watu wazima.

‎Alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 2020, chuo kimetoa wahitimu 57 katika ngazi mbalimbali na kukamilika kwa jengo jipya lenye thamani ya shilingi milioni 150 ni hatua muhimu ya kuimarisha miundombinu ya mafunzo na kuongeza mchango wake kwa jamii inayokizunguka.

‎Hafla hiyo ilihitimishwa kwa Prof. Sanga kuzindua rasmi mtaala mpya utakaoanza kutumika Machi 1, 2026 huku akikipongeza chuo kwa kuwekeza katika elimu inayoongeza maarifa, stadi na uwezo wa kujitegemea kwa wanajamii kwa ujumla. Alisisitiza lengo la kuanzisha chuo si kuhudumia wanafunzi wa ABC pekee, bali kuwa kitovu cha maarifa kitakachochochea maendeleo ya jamii nzima.