SERIKALI INAENDELEA KUWEKEZA KATIKA ELIMU YA WATU WAZIMA - PROF. MUSHI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika kukuza elimu jumuishi, mbadala na endelevu, hususan kwa wananchi waliokosa fursa ya elimu katika mfumo rasmi.
Prof. Mushi amesema hayo Disemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya 64 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea uwezeshaji wa wananchi kielimu, kiujuzi na kiakili.
Prof. Mushi ameipongeza TEWW kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Programu ya Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA), pamoja na maboresho ya mitaala inayozingatia mafunzo ya amali, stadi za maisha, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, aliwataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuongeza ufanisi katika taaluma zao, kutoa huduma kwa uadilifu, utu na haki, pamoja na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii, huku akiwahimiza kuwa mabalozi wazuri wa Taasisi na wazalendo wa taifa, sambamba na kutoa shukrani za dhati kwa wahadhiri, wafanyakazi, wazazi, waajiri na wadau wote kwa ushirikiano wao uliowezesha mafanikio ya wahitimu hao.
Mahafali hayo ya 64 yameonesha matokeo chanya ya uwekezaji wa Serikali katika elimu ya watu wazima, sambamba na mchango wa TEWW katika kufanikisha dhana ya Elimu Bila Ukomo. Hatua hizi zinaendelea kufungua fursa za elimu, kuongeza ujuzi na kuchochea ushiriki mpana wa wananchi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa.