TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
SERIKALI KUIMARISHA ELIMU YA WATU WAZIMA NCHINI ?
SERIKALI KUIMARISHA ELIMU YA WATU WAZIMA NCHINI ?
29th Aug, 2025

SERIKALI KUIMARISHA ELIMU YA WATU WAZIMA NCHINI

‎Na Mwandishi wetu, Dar es salaam 

‎Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaendelea kuboresha na kuimarisha elimu ya watu wazima ili kuwezesha watanzania walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi.

‎Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) , Prof. Mkenda alisema Serikali inajivunia mafanikio makubwa na hatua mbalimbali za Taasisi hiyo katika kushughulikia utolewaji wa elimu hiyo.

‎Mkenda ameitaka Taasisi hiyo katika kuadhimisha miaka 50 ya mafanikio inatakiwa kutafakari juu ya kuimarisha mifumo ya utoaji elimu bila ukomo ikiwemo kufanya mapitio ya Sheria na Miongozo.

‎Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali itaendelea kusambaza miundombinu ya elimu nchini kote ambayo ni pamoja na kampasi za vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na shule ili kufanikisha upatikanaji wa elimu kwa wote.

‎Kwa upande wake Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga aliwasilisha maazimio manne ya kuboresha Taasisi hiyo, ikiwemo; kuandaa waraka maalumu kwa wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari waliokosa fursa ya kuendelea, ili waweze kupata elimu nje ya mfumo rasmi.

‎Kuweka Kituo Jumuishi cha Ujifunzaji Jamii katika kila kata, kwa ajili ya mafunzo mbalimbali yatakayoongeza ujuzi na maarifa kwa wananchi.

‎Prof. Sanga alisisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio hayo utaongeza ubunifu na kuhakikisha elimu inawafikia watu wengi zaidi, hususan waliokosa nafasi kwenye mfumo wa kawaida wa elimu.

‎Katika maadhimisho hayo, kulifanyika maonesho ya kielimu, mijadala ya kitaalamu, maonesho ya kazi na bunifu za wahitimu wa programu za elimu ya watu wazima, pamoja na burudani kutoka kwa vikundi vya sanaa. Hafla hiyo imekuwa jukwaa la kuonesha mafanikio ya taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake kwa sheria ya Bunge Na. 12 ya mwaka 1975.