Na Mwandishi wetu, Morogoro
Serikali imeipongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia Baraza la Wafanyakazi na kuonesha mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Aidha, imeitaka taasisi hiyo kusimamia kwa karibu miradi ya IPOSA na SEQUIP-AEP ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa uwazi na kutoa matokeo yanayopimika.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa ElimuMsingi, Bw. Abdul Maulid, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Wafanyakazi wa TEWW unaofanyika Februari 19–20, 2026, Morogoro. Ameeleza kuwa kupitia IPOSA zaidi ya vijana 12,000 wamenufaika na programu za muda mrefu na zaidi ya 30,000 za muda mfupi, huku SEQUIP-AEP ikiandikisha wasichana 13,272 waliokatiza masomo, sawa na asilimia 111 ya lengo.
Serikali pia imeelekeza kukamilishwa kwa wakati miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, sambamba na kuoanisha mipango ya taasisi na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Hatua hizo zinalenga kuimarisha mchango wa TEWW katika kukuza rasilimali watu na uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga, ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kimkakati linalolenga kutathmini kwa kina utekelezaji wa maazimio yaliyopita na kuweka dira mpya ya vipaumbele vya taasisi. Akiwa kiongozi mwenye maono na msisitizo wa uwajibikaji, Prof. Sanga amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa wafanyakazi ni nguzo kuu ya mafanikio ya TEWW.
Mkutano huo unawakutanisha wajumbe 79 wanaowakilisha wafanyakazi 401 kutoka mikoa yote ya Tanzania, ukijadili masuala ya taaluma, fedha, mipango, utawala pamoja na mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.