BARIADI, SIMIYU, SEPTEMBA 25, 2026 - Serikali imeendelea kuweka fursa za Elimu Bila Ukomo na elimu nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuwawezesha watanzania kupata maarifa, ujuzi na stadi zinazowaongezea uwezo wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kisomo Kimataifa na Juma la Elimu Bila Ukomo Kitaifa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema elimu na ujuzi ni msingi wa kuongeza tija na ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi.
Prof. Mushi amesema Elimu Bila Ukomo, ikiwemo Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, inapaswa kuwafikia wananchi ambao hawakupata fursa ya kupata maarifa na ujuzi unaohitajika, ili waweze kujiletea maendeleo na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema TEWW inaendelea kutekeleza programu mbalimbali, ikiwemo Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA), unaowawezesha vijana kupata elimu, ufundi wa awali, ujasiriamali na stadi za maisha. Katika Mkoa wa Simiyu, vijana takribani 498 walidahiliwa katika awamu ya kwanza katika halmashauri za Busega, Bariadi Mjini, Maswa na Meatu.
Prof. Sanga amesema asilimia 25 ya watu wazima mkoani Simiyu hawana stadi za kusoma na kuandika, akisisitiza umuhimu wa kutumia takwimu hizo kupanga programu maalum za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa kisomo. Amewataka wananchi kutumia fursa za elimu zinazotolewa na Serikali, huku TEWW ikiendelea kushirikiana na halmashauri na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu, maarifa na stadi zinawafikia Watanzania wote ili kukabiliana na kiwango cha chini cha kisomo.