Na Mwandishi wetu, Shinyanga
Wadau wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi wamekutana kujadili utekelezaji wa Programu ya IPOSA ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha upatikanaji wa mafunzo ya ujuzi wa vitendo kwa vijana ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Akifungua mkutano wa Kamati ya Uratibu wa Programu hiyo uliofanyika Machi 11, 2026, Mkoani Shinyanga, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, alisema kuwa ingawa utekelezaji wa programu ulianza kwa kuchelewa kwa sababu mbalimbali, mradi umeonyesha mafanikio makubwa katika maeneo yote ya utekelezaji.
Prof. Sanga alieleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa karakana 27 za mafunzo ya ufundi stadi katika mikoa sita inayotekeleza programu hiyo pamoja na karakana tatu za mfano zilizopo katika mikoa ya Shinyanga, Manyara na Tanga. Alibainisha kuwa miundombinu hiyo ni muhimu katika kupanua fursa za vijana kupata mafunzo ya ujuzi wa vitendo.
Aidha, alisema kuwa tayari vifaa vya kufundishia vimepatikana ili kuwezesha utoaji wa mafunzo katika fani za ufundi ikiwemo ushonaji, utengenezaji wa batiki na uchomeleaji. Aliongeza kuwa uwepo wa wanafunzi wanaojiunga na mafunzo hayo unaonyesha uhitaji mkubwa wa vijana kupata ujuzi wa vitendo unaoendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 (Toleo la 2023) na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), Soyoung Park, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira thabiti katika utekelezaji wa Programu ya IPOSA, hususan katika ujenzi wa karakana 27 katika mikoa yote ya utekelezaji na karakana tatu za mfano. Aliongeza kuwa miundombinu hiyo inalenga kuimarisha ujuzi wa vijana, kuongeza ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo, na kuendeleza ujifunzaji kwa makundi mbalimbali ya wananchi, ili kuwasaidia vijana kupata stadi zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, OWM – TAMISEMI, TEWW pamoja na Maafisa Elimu EWW/EMNR kutoka mikoa sita ya utekelezaji. Aidha, mkutano umehudhuriwa pia na wadau wa maendeleo UNICEF na KOICA wanaoshirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mradi wa IPOSA.