Dar es Salaam, 7 Septemba 2026 - Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuwawezesha vijana kupata elimu, ujuzi na fursa za kujiajiri, hususan vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Bi. Jenifa Christian Omolo, ameipongeza TEWW kwa mchango wake katika kuwawezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu. Amesisitiza umuhimu wa kuwapatia vijana fani na ujuzi unaowawezesha kujiajiri, badala ya kutegemea ajira pekee, pamoja na kuwaunganisha na fursa za mikopo na mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga, ametaja maeneo ambayo TEWW inaweza kushirikiana na wizara hiyo, ikiwemo kuwawezesha vijana kupata ujuzi na stadi za kujitegemea, kuwajengea uwezo vijana na makundi ya uzalishaji mali, pamoja na kutambua vijana kulingana na ujuzi walionao. Aidha, ametaja utafiti na ubunifu kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano katika kubaini changamoto za vijana na kuandaa afua zinazozingatia matokeo ya tafiti.