TEWW YABORESHA MODULI ZA MKONDO WA JUMLA NA AMALI KUENDANA NA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO
Na Mwandishi wetu, Morogoro, Morogoro
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), kupitia Mradi wa SEQUIP–AEP, imeboresha moduli za masomo manane ya mkondo wa jumla na kuandaa mihtasari pamoja na moduli za masomo ya amali kwa hatua ya I (kidato cha kwanza hadi cha pili) cha elimu ya sekondari kwa njia mbadala. Hatua hiyo inalenga kuboresha mitaala ya elimu nje ya mfumo rasmi ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, inayosisitiza mafunzo ya amali.
Akifungua warsha hiyo Desemba 30, 2025, mkoani Morogoro, Mkuu wa TEWW Prof. Philipo Sanga alisema kazi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii kwani inawalenga Watanzania wengi walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu. Alieleza kuwa tangu awali TEWW imejikita katika utoaji wa elimu inayozingatia maarifa na ujuzi wa vitendo.
Prof. Sanga aliongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanafunzi laki nne hudondoka katika elimumsingi kila mwaka, hali inayowanyima fursa ya kuendelea na elimu katika mfumo rasmi. Alisema TEWW ilianzishwa kuwahudumia makundi hayo kwa kutoa elimu mbadala inayowawezesha kupata maarifa na ujuzi unaolingana na mfumo rasmi.
Alisisitiza kuwa maandalizi ya moduli hizo yanafanywa kwa kushirikisha wataalamu wenye sifa na uzoefu ili kuhakikisha zinamwezesha mwanafunzi kujitegemea au kurejea katika mfumo rasmi wa elimu.
Warsha hiyo ilianza tarehe 29 Desemba 2025 na itahitimishwa tarehe 2 Januari 2026, ikiwakutanisha wataalamu wa elimu ya sekondari, elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi. Lengo ni kupitia moduli za mkondo wa jumla na kuandaa moduli mpya za mkondo wa jumla na amali ili kuendana na sera husika.