TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YABORESHA UJUZI KWA MAAFISA USAFIRISHAJI NA MAMA LISHE
TEWW YABORESHA UJUZI KWA MAAFISA USAFIRISHAJI NA MAMA LISHE
13th Aug, 2025

TEWW YABORESHA UJUZI KWA MAAFISA USAFIRISHAJI NA MAMA LISHE

Na Mwandishi wetu, Mbeya

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imeendesha mafunzo maalum kwa maafisa usafirishaji na mama lishe mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Mafunzo hayo yamelenga kuongeza ujuzi katika ujasiriamali, elimu ya fedha, usalama barabarani, afya, utunzaji wa mazingira na uraia mwema, kwa lengo la kujenga jamii yenye maarifa, nidhamu na ustawi endelevu.

Akifungua mafunzo hayo leo Agosti 12, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, alisema kuwa maafisa usafirishaji na mama lishe ni sehemu muhimu ya uchumi wa taifa.

Mafunzo haya yawasaidie kuendesha biashara zenu kwa usalama, uadilifu na usafi, huku mkiona umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kufanya kazi kwa malengo. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuendelea kujifunza na kujiendeleza, kwa sababu elimu haina mwisho,” alisema Mhe. Itunda.

Alipongeza TEWW kwa kuchagua Mbeya kuwa sehemu ya kampeni hii ya kitaifa na kusisitiza kuwa elimu ya watu wazima ni hitaji la msingi katika karne ya sasa, si jambo la hiari tena.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Philipo Sanga, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya pili ya kujifunza, hususani wale waliopoteza fursa ya elimu ya awali.

“Takwimu zinaonesha asilimia 12.1 ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya hawana stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu. Tunawaomba tushirikiane kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma. Mali bila daftari hupotea bila habari, na elimu ndiyo msingi wa biashara endelevu,” alisema Prof. Sanga.

Prof. Sanga aliongeza kuwa moja ya malengo makuu ya mafunzo hayo ni kuwakumbusha maafisa usafirishaji umuhimu wa uendeshaji salama, ili kutokomeza kabisa ajali zinazopoteza nguvu kazi ya taifa. Alitaja takwimu za mwaka 2024 ambapo ajali 1,735 ziliripotiwa, kati yake 435 zikihusisha bodaboda.

Baadhi ya washiriki walipongeza TEWW kwa fursa hiyo, wakisema elimu waliyoipata itawawezesha kuboresha biashara na maisha yao. Waliomba serikali iendelee kuwafikia, kwani wengi wao hufanya maamuzi bila maarifa sahihi kutokana na ukosefu wa elimu.

Mafunzo haya, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yamehusisha takribani washiriki 200 wakiwemo maafisa usafirishaji na mama lishe toka Jiji la Mbeya ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW, ambayo kilele chake kitaadhimishwa tarehe 25 hadi 27 Agosti 2025.