TEWW YAFANYA MAHAFALI YA 64, YAIMARISHA DHANA YA ELIMU BILA UKOMO
Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imeandika historia nyingine kwa kufanya mahafali yake ya 64 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Desemba 17, 2025.
Mahafali hayo yameelezwa kuwa kielelezo cha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kukuza elimu jumuishi, mbadala na endelevu, hasa kwa wananchi waliokosa fursa ya elimu katika mfumo rasmi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu, Profesa Daniel Mushi, alisema kuwa mahafali hayo ni ushahidi wa wazi wa msimamo thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha elimu inakuwa haki ya msingi kwa kila Mtanzania.
"Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu bila ubaguzi, kwa kutambua kuwa maendeleo ya taifa yanategemea uwezeshaji wa wananchi wake kielimu, kiujuzi na kiakili bila kujali walipoanzia,” alisema Prof. Mushi.
Prof. Mushi aliipongeza TEWW kwa utekelezaji madhubuti wa programu na miradi mbalimbali, ikiwemo Programu ya Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA), pamoja na maboresho ya mitaala inayolenga zaidi mafunzo ya amali, stadi za maisha, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia, sambamba na mwelekeo wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo.
Kwa upande wake, Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga, alisema mahafali hayo yalihusisha jumla ya wahitimu 2,223 kutoka kampasi za Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza, waliotunukiwa vyeti na tuzo mbalimbali katika ngazi tofauti za mafunzo.
“Wahitimu hawa ni rasilimali muhimu kwa taifa. Kupitia elimu waliyoipata, wana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii zao,” alisema Prof. Sanga.
Aliongeza kuwa TEWW itaendelea kubuni na kuimarisha programu zinazolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan makundi yaliyo nje ya mfumo rasmi wa elimu, ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.
Serikali imeendelea kuimarisha TEWW kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuifanya kuwa nguzo ya “Elimu Bila Ukomo” kwa maendeleo endelevu ya taifa na ustawi wa jamii.