TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAFANYA TATHMINI YA MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA SEQUIP–AEP
TEWW YAFANYA TATHMINI YA MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA SEQUIP–AEP
02nd Mar, 2026

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, leo Februari 16, 2026, amefungua rasmi warsha ya siku tatu ya kutathmini utekelezaji wa mradi wa SEQUIP–AEP inayofanyika Kampasi ya Morogoro kuanzia Februari 16–18, 2026. Warsha hiyo imewakutanisha wasimamizi na watekelezaji wa mradi huu kutoka nchi nzima kwa lengo la kufanya tathmini ya kina, kubaini mafanikio na changamoto, pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji.

Akifungua warsha hiyo, Prof. Sanga alieleza kuwa tathmin hiyo ni sehemu ya wajibu wa taasisi katika kusimamia mradi wa uboreshaji wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala. Alisisitiza kuwa siku hizo tatu ni fursa muhimu ya kujipima, kujifunza na kupanga mikakati itakayoongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Warsha hiyo inalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa SEQUIP–AEP, kuwajengea uwezo washiriki kupitia mafunzo ya usimamizi wa mradi na matumizi ya mfumo wa OSMIS, pamoja na kutekeleza kazi za kiufundi zikiwemo uingizaji na uhakiki wa takwimu katika mfumo rasmi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha utendaji wa taasisi kwa ujumla, si katika mradi pekee bali pia katika majukumu mengine ya kitaasisi.

Katika tathmini yake, Prof. Sanga alibainisha kuwa mradi umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu kama madarasa, mabweni na majengo ya utawala katika mikoa mbalimbali, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaofaulu na kuendelea na masomo. Alihitimisha kwa kusema kuwa TEWW itaendelea kuishauri Serikali kwa kutumia uzoefu na matokeo ya utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya jamii.