TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAIMARISHA MAFUNZO YA AMALI KWA VIJANA KUPITIA IPOSA NA MFUMO WA TUZO NDOGO
TEWW YAIMARISHA MAFUNZO YA AMALI KWA VIJANA KUPITIA IPOSA NA MFUMO WA TUZO NDOGO
23rd Mar, 2026

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

‎Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema taasisi hiyo imeendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya amali kwa vijana nchini ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kuchangia pato la  taifa.

‎‎Prof. Sanga amebainisha hayo jijini Dar es Salaam leo Machi 23, 2026 wakati wa mahojiano yaliyorushwa mbashara na kituo cha UFM radio.

Kulingana na kiongozi huyo, TEWW imepata msukumo zaidi katika jitihada zake kufuatia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) inayotilia mkazo mafunzo ya amali.

Kupitia Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (MECHAVI), TEWW imekuwa ikitoa mafunzo kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu katika mikoa 16, ambapo takriban vijana 42,000 tayari wamenufaika kwa kupata ujuzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya maeneo yao na soko la ajira, Prof. Sanga amesema.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa IPOSA unaofanyika katika mikoa sita (6) ya Manyara, Tanga, Shinyanga, Simiyu, Singida na Pwani  imejenga jumla ya karakana 31 zenye vifaa vya kisasa na wawezeshaji mahiri.

Katika mikoa hiyo sita takriban vijana 3,285 wanatarajiwa kudahiliwa na kupatiwa mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kuingia moja kwa moja kwenye shughuli za uzalishaji mali, Mkuu huyo wa Taasisi amesema.

‎‎Aidha, amebainisha kuwa TEWW imeanzisha mfumo wa mafunzo wa “tuzo ndogo ndogo” (micro-credentials system) unaolenga kutoa stadi kwa muda mfupi wa miezi mitatu mitatu, hatua inayomwezesha kijana kupata ujuzi wa haraka na kuanza kujiajiri kabla ya kuendelea na hatua nyingine za mafunzo.