Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka misingi imara inayowawezesha vijana kupata ujuzi na maarifa muhimu kwa maisha yao, hatua inayoiwezesha TEWW kupanua fursa za mafunzo ya amali kwa vijana nchini.
Akizungumza leo, Machi 18, 2026, katika kipindi cha Baragumu Live kinachorushwa na Channel Ten jijini Dar es Salaam, Prof. Sanga alieleza kuwa Taasisi hiyo inalenga kutoa elimu jumuishi kwa watu wa rika zote, bila kujali umri, hali au mazingira waliyopitia.
Prof. Sanga alifafanua kuwa TEWW inaelekeza nguvu zake zaidi kwa vijana walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu, wakiwemo wale waliolazimika kuingia katika majukumu ya utu uzima mapema kutokana na sababu mbalimbali.
“Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha mfumo wa elimu ili ukidhi mahitaji ya sasa kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023). Kupitia sera hiyo, vijana wanapata fursa ya kujifunza mafunzo ya amali ambayo yanaendana moja kwa moja na mahitaji ya soko la ajira,” alisema Prof. Sanga.
Kwa zaidi ya miaka 50, TEWW imeendelea kusimama imara katika utekelezaji wa dhamira yake ya kutoa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, hatua inayofungua milango ya matumaini mapya kwa vijana na watu wazima kote nchini. Kupitia programu zake zinazotolewa kuanzia ngazi ya Elimu msingi hadi Shahada ya Uzamili, Taasisi hiyo imeendelea kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya rasilimali watu, ikiandaa wahitimu wenye ujuzi na uwezo wa kukabiliana na soko la ajira.