TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAKUSANYA MAONI YA WADAU KUBORESHA MITAALA YA MAFUNZO YA AMALI
TEWW YAKUSANYA MAONI YA WADAU KUBORESHA MITAALA YA MAFUNZO YA AMALI
30th Mar, 2026

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Sanga, amesema lengo kuu la taasisi ni kuandaa wakufunzi wenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uboreshaji wa mitaala, ili kuijenga jamii yenye ujuzi, maarifa na mtazamo chanya na kuzalisha matokeo yanayokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Amebainisha hayo wakati akifungua warsha ya wadau iliyolenga kupitia na kukusanya maoni ya maboresho ya mitaala leo, Machi 30, 2026 Makao Makuu ya TEWW jijini Dar es Salaam, Prof. Sanga amesema TEWW inathamini ushiriki wa wadau, akisisitiza kuwa inasaidia kuandaa programu zinazojibu changamoto za jamii.

Ameeleza kuwa mafunzo ya amali yanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu, hali inayochochea jitihada za serikali na wadau kutafuta suluhisho. Amesema TEWW imeanzisha programu za kuandaa wawezeshaji ili kujenga uwezo wa ndani unaokidhi mahitaji ya sasa.

Vilevile, amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kutoa mawazo yatakayosaidia kuboresha nyaraka za mitaala, akisisitiza kuwa taasisi ina matarajio makubwa ya kupata matokeo yatakayotekelezeka na yenye tija.

Warsha hiyo ilihudhuliwa na wadau mbalimbali, wakiwemo NACTVET wataalamu wa ufundi kutoka VETA, DIT, NIT, CBE na Taasisi ya Ustawi wa Jamii; wanafunzi na wanataaluma kutoka TEWW.