TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAKUTANA NA WADAU NA WAMILIKI WA SHULE HURIA DAR ES SALAAM
TEWW YAKUTANA NA WADAU NA WAMILIKI WA SHULE HURIA DAR ES SALAAM
15th Apr, 2026

Aprili 14, 2026, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imekutana na wadau wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi pamoja na wamiliki wa shule huria katika kikao kazi kilicholenga kujadili na kuboresha utekelezaji wa elimu mbadala nchini.

‎Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Mkuu Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (Mipango, Fedha na Utawala), Dkt. Honest Kipasika kwa niaba ya Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga wamewataka wadau hao na wamiliki kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha huduma za elimu mbadala nchini.

‎Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi huyo alisisitiza juu ya umuhimu wa kila mdau kuelewa mipaka ya majukumu yake ili kuondoa migongano ya kiutendaji na kuongeza ufanisi.

‎Kikao hicho kilijadili mada muhimu zikiwemo rasimu ya uendeshaji wa shule huria na elimu ya watu wazima, mtihani wa utamilifu (mock exam), pamoja na mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi (SEQUIP).

‎Kikao hicho cha siku moja kiliwashirikisha viongozi na wataalamu wa elimu kutoka ngazi ya mkoa na halmashauri; wathibiti ubora wa shule; waratibu wa mradi wa vituo vya SEQUIP; maafisa kutoka TEWW pamoja na wamiliki wa shule huria mkoani Dar es Salaam.