TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAMPONGEZA NA KUMUAGA RASMI MH. ASHA FERUZI
TEWW YAMPONGEZA NA KUMUAGA RASMI MH. ASHA FERUZI
23rd Mar, 2026

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imempongeza na kumuaga rasmi aliyekuwa mtumishi wake, Mh. Asha Feruzi (MB), Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vyuo na vyuo vikuu, kufuatia utumishi wake uliotukuka uliotawaliwa na uadilifu, ubunifu na kujituma.

Hafla hiyo iliongozwa na Mkuu wa Taasisi, Prof. Philipo Sanga, ambaye kwa niaba ya Menejimenti na watumishi alisema TEWW inajivunia mafanikio ya Mh. Feruzi, akibainisha kuwa mchango wake umeacha alama ya heshima na maendeleo ndani ya taasisi.

“Umetuachia urithi wa mafanikio; tunaamini utaendelea kuwa balozi mwema wa TEWW popote utakapokuwa,” alisisitiza Prof. Sanga.

Katika kuthamini mchango wake, TEWW ilimkabidhi Mh. Feruzi cheti cha pongezi pamoja na zawadi maalum kama ishara ya kutambua utumishi wake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mh. Asha Feruzi, ambaye pia aliwahi kuwa Mhadhiri Msaidizi wa TEWW, alitoa shukrani kwa uongozi na watumishi kwa ushirikiano na mazingira bora ya kazi. Aidha, alihimiza taasisi kuendelea kupanua wigo wa elimu kwa kuimarisha na kutangaza kozi za muda mfupi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Taasisi (Mipango, Fedha na Utawala), Dkt. Honest Kipasika, alisema TEWW itaendelea kujivunia mchango wake na kudumisha ushirikiano, huku akisisitiza kuwa Mh. Feruzi ataendelea kuwa sehemu ya familia ya TEWW.