TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAPANUA FURSA ZA ELIMU NA UJUZI KWA VIJANA NCHINI
TEWW YAPANUA FURSA ZA ELIMU NA UJUZI KWA VIJANA NCHINI
23rd Mar, 2026

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi, ikiwa ni jitihada za kuwafikia vijana na watu wazima waliokosa au waliodondoka katika mfumo rasmi wa elimu kwa sababu mbalimbali, sambamba na kupanua fursa za mafunzo ya ujuzi kwa vijana nchini.

Akizungumza leo, Machi 19, 2026, katika kipindi cha Helo Tanzania kinachorushwa na Uhuru FM, Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Philipo Sanga, alisema kuwa TEWW inatekeleza majukumu yake katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, kwa lengo la kuhakikisha hakuna mwananchi anaekosa fursa ya elimu.

Prof Sanga, alibainisha kuwa TEWW pia ni chuo cha elimu ya juu kinachotoa mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Shahada ya Uzamili katika kampasi zake zilizopo Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Ruvuma, kwa lengo la kuandaa wataalamu wa kusimamia elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini.

"Juhudi hizo za utoaji mafunzo ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Tawala Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), ambazo kwa pamoja zinalenga kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na kuongeza ajira kwa vijana". Alisema Prof. Sanga

Aliongeza kuwa TEWW inatekeleza mkakati unaojumuisha utoaji wa stadi za kisomo, stadi za maisha, ujasiriamali na ufundi wa awali ili kuwezesha vijana
kupata mafunzo ya muda mfupi yatakayowawezesha kujiajiri au kuajirika kwa haraka kulingana na mahitaji ya soko la ajira, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa vijana katika maendeleo ya uchumi wa taifa.