TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAPANUA FURSA ZA MAFUNZO YA AMALI; KARAKANA YA IPOSA YAKABIDHIWA KISHAPU
TEWW YAPANUA FURSA ZA MAFUNZO YA AMALI; KARAKANA YA IPOSA YAKABIDHIWA KISHAPU
23rd Mar, 2026

Na Mwandishi wetu, Kishapu - Shinyanga

‎Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inaendelea kuimarisha juhudi za kuwapatia vijana waliokatisha masomo ujuzi wa amali kupitia utekelezaji wa mradi wa IPOSA, ambapo jengo la karakana ya mafunzo limekabidhiwa rasmi katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

‎Makabidhiano hayo yalifanyika Machi 13, 2026 katika Kijiji cha Negezi, Kata ya Ukenyenge, ambapo jengo hilo lililojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) lenye thamani ya shilingi milioni 57.9 lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ili kutumika kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, alisema taasisi inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa IPOSA nchini kwa lengo la kuwafikia vijana waliokosa fursa ya elimu na kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi. Alieleza kuwa mradi huo unaunganisha elimu ya msingi na mafunzo ya stadi ili kuwasaidia vijana kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika shughuli za uzalishaji na ajira binafsi.

‎Vilevile, amewataka wanafunzi wa mradi huo kujituma katika masomo yao ili kufikia malengo yao, huku akisisitiza kuwa serikali inahakikisha kila mwananchi anapata ujuzi na uwezo wa kujisimamia kiuchumi licha ya tofauti za majukumu.

‎Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Bw. Emmanuel Johnson, aliishukuru Serikali ya Tanzania, TEWW pamoja na wadau wa maendeleo kwa kuiletea wilaya hiyo mradi ambao unaleta matumaini mapya kwa vijana waliokatisha masomo yao, akibainisha kuwa karakana hiyo itasaidia kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi na kuwawezesha vijana kujiajiri.

‎Mradi wa IPOSA unalenga kuwapatia vijana wa kike na wa kiume walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu ujuzi wa fani mbalimbali ikiwemo ushonaji na mekanika, ambapo katika kituo hicho cha Kishapu jumla ya vijana 126 tayari wamejisajili kuanza mafunzo ya ufundi.