TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
TEWW YAZINDUA MAFUNZO YA UENDESHAJI WA VITUO VYA KISOMO
TEWW YAZINDUA MAFUNZO YA UENDESHAJI WA VITUO VYA KISOMO
07th Aug, 2025

TEWW YAZINDUA MAFUNZO YA UENDESHAJI WA VITUO VYA KISOMO

Urambo, Tabora 

‎Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe, Paul Chacha, aliewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamisi Mkanachi, Agosti 06, 2025 amezindua rasmi mafunzo ya uendeshaji wa madarasa ya kisomo yanayoendeshwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Margaret Sitta, Wilaya ya Urambo.

‎Uzinduzi huo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuimarisha hali ya kisomo nchini kupitia madarasa ya kisomo, ambapo kwa Mkoa wa Tabora, shughuli hii inalenga kukabiliana na changamoto ya watu wasiokuwa na stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK). Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 32% ya wakazi wa Tabora bado hawajapata ujuzi wa KKK, hali inayokwaza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

‎Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Mkanachi alitoa wito kwa viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mkakati wa Kisomo utakaoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

‎“Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inaandaa mkakati wa kitaifa wa kisomo utakaowasilishwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, hivyo ni wajibu wa kila kiongozi katika ngazi zote kuhakikisha kila mwananchi anapata stadi za kisomo,” alisema Dkt. Mkanachi.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Philipo Sanga, alisema TEWW imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata stadi za KKK kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kisomo wa kufufua na kuuisha vituo vya kisomo, hususani katika maeneo yaliyoathirika zaidi, ikiwemo Mkoa wa Tabora.

‎“Mpango huu utafikishwa kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya utekelezaji katika wilaya zote. Tabora ina takribani wakazi milioni 3.3 na asilimia 32% hawana stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu. Hili ni pengo kubwa katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Prof. Sanga.

‎Alibainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya ujinga, ikiwemo kuimarisha elimu nje ya mfumo rasmi kupitia programu za MUKEJA, IPOSA, pamoja na elimu ya sekondari kwa njia mbadala.

‎Prof. Sanga aliongeza kuwa mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na kilele chake ni tarehe 25–27 Agosti, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.