WAZIRI MKUU AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA ELIMU YA WATU WAZIMA
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kulingana na mahitaji ya sasa na baadaye.
Akizungumza leo Agosti 25, 2025 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Mhe. Majaliwa amesema teknolojia ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha elimu inawafikia Watanzania wengi zaidi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
Ameeleza kuwa Serikali inatambua changamoto zilizopo katika upatikanaji wa elimu kwa wote, na ndiyo maana imeweka msisitizo katika matumizi ya TEHAMA, ikiwemo mifumo ya kidijitali, mitandao ya simu na majukwaa ya kujifunzia mtandaoni, ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wadau wa elimu, taasisi binafsi na sekta ya umma kushirikiana na TEWW katika kuendeleza miundombinu na programu za kidijitali zitakazosaidia watu wazima na vijana waliokosa nafasi ya elimu ya kawaida kupata maarifa mapya.
Akiongea katika Kongamano hilo, Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga, amesema taasisi yake imejipanga kutumia teknolojia ya kisasa katika kufundisha ili kuhakikisha elimu inakuwa shirikishi, jumuishi na endelevu.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa hatua hii itasaidia kujibu mahitaji ya soko la ajira na kuendana na maendeleo ya dunia ya kidijitali, ambapo maarifa na ujuzi hupatikana kupitia mifumo rahisi na ya haraka.