WAZIRI MKUU ATOA PONGEZI KWA TEWW
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameipongeza Taasisi ya Watu Wazima (TEWW) kwa mchango wake mkubwa katika utoaji elimu nje ya mfumo rasmi na elimu ya watu wazima nchini.
Akifungua Kongamano la Elimu bila Ukomo kwa Maendeleo Endelevu kuadhimisha Miaka 50 ya TEWW leo Agosti 25, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Mhe. Majaliwa amesema kuwa mchango wa taasisi hiyo umeongeza uelewa na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Mhe. Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuiwezesha TEWW kwa kuipatia rasilimali stahiki ili wananchi wananchi waendelee kupata huduma bora ya elimu, ikiwemo mafunzo ya ufundi, ujuzi wa stadi za kazi, pamoja na elimu ya uraia inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini safari ya taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha mchango wake katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Taasisi Kongamano hilo la siku tatu limekusanya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo litajadili pamoja na mambo mengine mada mbalimbali kuhusu mustakabali wa elimu ya watu wazima, teknolojia katika ufundishaji, na mbinu za kukuza ushirikishwaji wa wananchi katika kupata mafunzo endelevu.