Na Mwandishi Wetu, Manyara
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa IPOSA unaoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kufuatia ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa karakana za mafunzo mkoani Manyara.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Kamishna wa Elimu Tanzania, Dkt. Lyabwene Mtahabwa, ilihusisha kukagua maendeleo ya ujenzi wa karakana na miundombinu ya vyoo katika halmashauri zinazotekeleza mradi huo: Halmashauri ya Mji wa Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Halmashauri ya Mji wa Mbulu, na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu.
Akizungumza wakati wa ziara, Dkt. Mtahabwa alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi na kuipongeza TEWW kwa usimamizi mzuri. Alisisitiza umuhimu wa kuwafikia vijana wengi zaidi ili kunufaika na fursa zinazotolewa kupitia mradi huo, akibainisha kuwa mafunzo ya ufundi na stadi za maisha ni nyenzo muhimu za kuwawezesha vijana kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga, alisema taasisi inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha karakana zinazojengwa zinakidhi malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi na stadi za maisha kwa vijana walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu. Aliongeza kuwa miundombinu hiyo itasaidia vijana kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri.